SERIKALI YAMKATIA RUFAA PADRE KIMARO by nasanyo fortnine

Mahakama ya Rufaa imeshindwa kusikiliza rufaa ya Jamhuri dhidi ya aliyekuwa padri wa kanisa Katoliki, Sixtus Kimaro, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na baadaye kuachiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Kushindwa kusikilizwa rufaa hiyo kulitokana na Kimaro kutokujulikana alipo kwa vile alishafukuzwa na Kanisa hilo kutoa huduma.

Kabla ya hatua hiyo, Wakili wa Serikali, Salum Malick alieleza kuwa wamepata taarifa kwamba  msajili wa mahakama hiyo kuwa  mhusika alipelekewa hati ya wito kwa mwajiri wake Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dar es Salaam, lakini  waliambiwa kuwa kwa sasa Padri Kimaro siyo mwajiriwa wao tena na kwamba hawajui mahali alipo.

Padri Kimaro alihukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya msingi namba 786 ya mwaka 2005, Alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu, yakiwamo ya kumlawiti kijana wa miaka 17,  shambulio la aibu na kumdhalilisha mtoto huyo.

Padri huyo alikamatwa na askari Polisi wa doria Mei 18, 2005, usiku katika eneo la Changanyikeni, Dampo jijini Dar es Salaam.Aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo,  Pelagia Khaday, Agosti 9, 2006, alimtia hatiani Padri Kimaro.

Padri Kimaro baada ya kupatikana na hatia katika makosa yote alihukumiwa adhabu ya kifungo cha  miaka 35 jela.Katika kosa la kwanza alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na  katika kosa la pili alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 5 jela na akaamuriwa kumlipa fidia ya shilingi milioni mbili mtoto huyo.

Hata hivyo, Padri alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilisikilizwa na Jaji Robert Makaramba, akipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu.
Katika hoja zake alidai kuwa Jamhuri haikutoa ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Jaji Makaramba alikubaliana na rufaa hiyo na Machi 14, 2008, alimwachia huru akisema kuwa ameridhika kwamba hapatakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.

Jaji Makaramba alisema kuwa hitimisho lake katika hukumu yake kulingana na muda na mahali mjibu rufani na kijana huyo walikokutwa ni ushahidi wa kimazingira. Alisisitiza kuwa shahidi wa pili na wa tatu wa mashtaka (askari waliodaiwa kumkuta Padri Kimaro akitenda kosa hilo na kijana huyo) hawakueleza kwa uhakika kile ambacho mjibu rufani alikuwa akikifanya.

Jamhuri katika rufaa yake imewasilisha jumla ya hoja saba kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumwachia huru Padri Kimaro.Serikali imesema Jaji aliyesikiliza rufaa hiyo pia alikosea kisheria na kiukweli kueleza kuwa hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa nini mjibu rufani alikuwa  akifanya eneo la Dampo.

Imesema Jaji aliyesikiliza rufaa alikosea kisheria na kiukweli kwa kutotambua ushahidi wa shahidi wa nne katika mashtaka hayo bila kutoa sababu zenye nguvu na kwamba alikosea kisheria kwa uamuzi wake kuegemea kwenye ushahidi wa mazingira.

Adha, upande wa serikali umeeleza kuwa Jaji aliyesikiliza rufaa hiyo alikosea kisheria kueleza kuwa shahidi wa nne wa mashtaka na mjibu rufani walilazimishwa uchunguzi wa kitabibu  na kwamba fomu ya Polisi namba 3 (PF3) iliyowasilishwa mahakamani ilikuwa ni kusudi la utambuzi tu.

Serikali imesema Jaji alijipotosha mwenyewe kuhusiana na sheria inayohusu ushahidi wa kimazingira na kwamba  alikosea kisheria na kiukweli kusema kuwa hapakuwa na ushahidi wa kuunga mkono ushahidi wa shahidi wa nne.

Upande huo wa serikali ilieeleza kuwa Jaji aliyesikiliza rufaa alikosea kisheria na kiukweli kueleza kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG