KESI YA MAUAJI; MAJAJI WAWILI WAJITOA by nasanyo fortnine

Majaji wawili wajitoa kesi mauaji Profesa Mwaikusa

Aliyekuwa wakili maarufu na mwanazuoni nguli nchini, Professa Jwani Mwaikusa.
 
Majaji wawili wa Mahakama Kuu wamejitoa kwa nyakati tofauti kusikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa wakili maarufu na mwanazuoni nguli nchini, Professa Jwani Mwaikusa, inayowakabili washtakiwa wawili.

Hayo yalibainika jana baada ya Jaji Lawrence Kaduri kushindwa kusikiliza kesi hiyo na kuamua kujitoa ili kuepuka mgongano wa maslahi.
Jaji Kaduli aliyekuwa asikilize kesi hiyo hadi Julai 18, mwaka huu, alisema amekuwa na uhusiano wa karibu na marehemu na kwamba, wamesoma wote shule moja.

“Kwa misingi hiyo, siwezi kuendelea na shauri hili. Hivyo narudisha faili la kesi hii kwa jaji mkuu wa kanda ili liweze kupangiwa jaji mwingine wa kusikiliza,” alisema Jaji Kaduri.

Hii ni mara ya pili kwa jaji wa Mahakama Kuu kujitoa kwenye kesi hiyo, baada ya Jaji wa kwanza, Fauz Twaib, naye kufikia uamuzi huo kwa sababu kama hizo.

Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi itakapopangwa tena mbele ya jaji mwingine.Washtakiwa katika kesi hiyo ni Joseph Machoche na Jackson Zebedayo. Wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 13, 2010, maeneo ya Salasala, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mwaikusa ambaye pia alikuwa wakili wa kujitegemea na Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alikutwa na maafa hayo alipokuwa amewasili nyumbani kwake akitoka ofisini majira ya saa tatu usiku.

Wengine waliouawa kikatili pamoja na Profesa Mwaikusa ni kijana mwenye umri wa miaka 25, Gwamaka Mwasanjala, akitajwa kuwa ni mpwa wa marehemu Mwaikusa na mfanyabiashara John Mtui, ambaye ni jirani yao.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG