VITA YA TANZANIA NA MALAWI KIKWETE ANENA HAYA by nasanyo fortnine

by nasanyo fortnine
Rais Jakaya Kikwete
 
Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano wa mpaka kati yake na Malawi.

Alisema Tanzania haioni matinki yoyote ya kuingia vitani na nchi yoyote jirani.
Aliihakikishia nchi hiyo ya Malawi wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Michezo wa mjini Mbamba Bay, mji mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa, akiwa kwenye ziara ya mkoa wa Ruvuma.

Rais Kikwete ambaye alikuwa akizungumzia juhudi za kutafuta ufumbuzi wa suala la mpaka kati ya Tanzania na Malawi, aliwaondoa wasiwasi wananchi hao kwa kueleza kuwa hakuna sababu ya kuingia vita na nchi jirani.

 "Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita."

Alisema Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka.
“Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita.  Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya majadiliano.

Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi  pekee bali kwa mipaka yote ya Tanzania," alisema.

Aliwaeleza wananchi hao juhudi  zinazofanywa na Tanzania kutatua tatizo hilo la mpaka ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la marais wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la mpaka kati ya nchi hizo mbili.

Marais hao ni Joachim Chissano wa Mozambique, Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, wanaosaidiwa na jopo la Kimataifa la mabingwa wa sheria katika kazi  hiyo.

Aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa serikali kununua na kuweka meli mpya katika Ziwa Nyasa uko pale pale na kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha chelezo cha kujengea meli kutoka Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi, Kyela, Mbeya ili kuanza ujenzi wa meli hiyo.

Rais ambaye katika Kampeni ya Uchaguzi Mkuu Mwaka 2010 aliahidi ununuzi wa meli tatu za kutoa huduma katika maziwa makuu ya Tanzania ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, alisema kuwa kiasi cha Sh. bilioni 23 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli hiyo.

Alisema kuwa michoro ya meli hiyo ya Ziwa Nyasa imelazimishwa kubadilishwa kidogo kwa sababu ziwa hilo lina mawimbi makali na huchafuka mara kwa mara tofauti na Victoria na Tanganyika.

Aidha, alisema serikali inaendelea na mipango ya kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa Mtwara na kuweza kubeba chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma, maeneo yaliyoko katika mkoa wa jirani wa Njombe na wilaya jirani na Nyasa ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe.

Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma, alizindua Daraja la Ruhekei lililoko katika Kijiji cha Mkalole, kilomita nane kutoka mjini Mbamba Bay.

"Ni kweli Mwaka 2005 wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu nilishindwa kuvuka hapa kwa sababu daraja lilivunjika lakini ujenzi huu wa kisasa ni kwa sababu tunajiandaa kujenga barabara ya lami kuunganisha Mbinga na Mbamba Bay," alisema.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG