SUMAYE;CCM NJIA PANDA UCHAGUZI 2015 HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo fortnine

Rushwa kuiweka CCM njiapanda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kipo hatarini kukumbwa na mpasuko mkubwa pindi chama hicho kitakapomsimamisha mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambaye anapenda vitendo vya rushwa.

Hali hiyo inadhihirishwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye, ambaye ameweka wazi kwamba atakihama chama hicho endapo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 atasimamishwa mgombea anayependa vitendo vya rushwa.

Sumaye aliyasema hayo jana wakati akihojiwa katika kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi, kilichorushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha Star TV.

Alisisitiza kuwa mtu anayetoa rushwa hawezi kuwatumikia wananchi, hivyo yeye atahama CCM endapo kwenye Uchaguzi wa Mkuu wa mwaka 2015 atasimamishwa mgombea anayependa vitendo vya rushwa.

Alisema, siasa za Tanzania kwa sasa zimekuwa fedha kwani kama mtu huna fedha huwezi kuchaguliwa; jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya nchi na tusipoangalia basi nchi itapata anguko kubwa.

Sumaye alisema kama utaratibu huo utaendelea wa kwamba mwenye fedha ndiye anaongoza nchi, basi Watanzania wajiandae kuumia, kwani mtu huyo anakuwa hana machungu na nchi yake, mwishowe ataongoza nchi kwa kutumia rimoti, ambapo ikiwa amepewa sh. milioni 10 za kufanyia kampeni na akawa kiongozi sasa huyo mtu atawezaje kumshurutisha alipe kodi? Matokeo yake ni wenye fedha ndio wataendesha Serikali.

Alisema endapo mtu ana vigezo vya kuwa kiongozi, basi haina haja ya kutoa ruswa, kwani wananchi wenyewe ndio wanaona utendaji wake."Hata wananchi wanajua kuwa mtu akiingia madarakani kwa kutoa rushwa anakuwa hana moyo wa kuwatumikia, bali anajali masilahi yake binafsi," alisema Sumaye na kuongeza;

"Siwezi kuwakataza wananchi kuchukua fedha watakazopewa na wagombea wachukue, lakini wasiwachague,tukifanya hivyo vitendo vya rushwa vitapungua."

Alisema, Serikali nyingi duniani zimeanguka kwa mfumo huo na kwamba kama hali hiyo itaendelea nchini, CCM itakufa. Aliongeza kwamba;

"Mtu kama unajiona wewe ni mrefu kwa nini uongeze tofali,mtu huyo anaweka tofali ili aweze kuvifikia virefu wakati hana sifa za kufika atakapo, hata hawa viongozi watoa rushwa ndio walivyo hawana vigezo lakini wanataka kulazimisha wafike wanapotaka."

Alifafanua kwamba; "Jamii ina hasira,jiulize kwa nini watu hawachomi boda boda na wakati huo wanaenda kuchoma gari la mbunge, ni kwamba watu wamechoka na matabaka yanayowekwa na viongozi."

Alisema njia mojawapo ya kukomesha rushwa ni kutomchagua anayetoa hongo na kuonya kwamba kama vitendo hivi vitaendelea basi hata CCM kitapata pigo na nchi yenyewe itaenda mrama.

Aliongeza kuwa, uchumi wa Tanzania uko kwenye mikono ya watu wachache, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya nchi na kumtaka Rais anayekuja aangalie jinsi ya kulitatua hilo tatizo.

"Anayetakiwa kulipa kodi, basi alipe kodi ili pawepo na usawa kati ya wenye nacho na wasio kuwa nacho," alisema Sumaye.

.Akiongelea suala la mgombea urais kwa mwaka 2015, alisema ujana na uzee si sifa ya mtu kuwa rais bali kinachotakiwa ni mtu kuwa na vigezo vya kuweza kuongoza Taifa.

"Kama tunamwona an a nguvu,maadili, mchapakazi na anatetea masilahi ya Taifa, basi tumchague lakini si kigezo cha wewe ni mzee au kijana ndio tukupe nafasi wakati huna vigezo,"alisema Sumaye.

Alisema suala la Rais kutakiwa kuwa kijana au mzee lisiwapotezee muda watu, kwani suala hilo linataka kuwaondoa kwenye ajenda ya msingi ya kupata Rais anayefaa.

"Sifa za urais zipo na ili mtu agombee lazima jamii ikuone unafaa na una kila kigezo kwa hiyo mambo ya sijui rais awe kijana au mzee lisitupotezee muda, kwani litatuondoa kwenye hoja ya msingi,"alisema Sumaye.

Alisema katika utawala wa awamu ya tatu Serikali ilibana sana matumizi ya Serikali, hali iliyosaidia nchi kuwa na fedha za kutosha na kusababisha kudai kuwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ameficha fedha nje ya nchi.

"Mimi nilichapa kazi kweli kweli kwa kuwa ndio nilikuwa msimamizi mkuu na tangu niteuliwe nafasi ya Waziri Mkuu kwa miaka 10 sikuwahi kwenda likizo, hivyo muda ukifika nitagombea au sitagombea na nikiwa rais au nisiwe rais nitaendeleza mapambano dhidi ya rushwa," alisema Sumaye. 

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG