WANANCHI WAPIGA HADI KUUA AFISA MIFUGO HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo fortnine

Benedict Kitenga
 
Watu  watatu akiwamo afisa kilimo na mifugo wa Kata ya Rwabwere Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera waliouawa kwa kushambuliwa na  wananchi wakidhaniwa majambazi, wanatarajiwa kuzikwa leo.

Kulingana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Benedict Kitenga watu hao waliuawa na wakazi wa Kijiji cha Kalongo Kata ya Rwabwere  usiku wa kuamia Aprili 12, mwaka huu.

Kitenga alisema kuwa miili ya watu hao, Shimbwilo Jonathan (44), Juma Mbogo (48), wakazi wa kijiji Kitale na ofisa huyo, Jacknus Wamala imehifadhiwa katika Zahanati ya Nkwenda.

Alisema  siku ya tukio hilo, watu hao wakiongozwa na afisa kilimo huyo walifanya msako wa kuwatafuta ng’ombe 12 walioibwa kutoka kijiji chao cha Kitale kipindi cha wiki moja iliyopita.

Alisema walipofika katika kijiji cha Kalongo waliwapata ng’ombe hao wakiwa nyumbani kwa Joas Agustino na kumkamata kisha kuondoka naye usiku huo kwa lengo la kumkabidhi katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.

Alisema baada ya kumchukua mtuhumiwa huyo, mkewe alipiga yowe na ngoma ya kuashiria hatari.

Alisema  baadhi ya wakazi  wa kijiji cha Kalongo waliamka kutoa msaada.

Kitenga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, alisema baada ya kuamka mke wa Agustino aliwaeleza kuwa mmewe ametekwa na majambazi na kuondoka naye.

Alisema baada ya wakazi hao  kuelezwa hivyo walianza kuwafuatilia na kuwakamata wakati wakielekea katika kijiji chao na mtuhumiwa huyo na kuwashambulia kwa silaha za jadi ikiwamo mapanga na kuwaua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Kagera, George Mayunga amekiri kutokea kwa mauaji hayo na kwamba wanawashikilia watu wanne kwa kuhusika nayo.

Alisema bado wanaendelea kufanyamsako mkali dhidi ya wengine waliojichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watu hao.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG