MWL.. MKUU AKATWA MAPANGA NA WANAFUNZI WAKE HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo..fortnine

Bunda. Wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Kibara, wilayani
 Bunda  wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Bunda
 wakikabiliwa na shtaka la kumshambulia na kumjeruhi kwa panga mwalimu
 mkuu wa shule hiyo.
Ilielezwa kuwa wanafunzi hao walimjeruhi mwalimu huyo baada ya kutaka
 kurejeshewa fedha zao za ada kwa vile hawakuwa na mpango tena wa kuendelea
 na masomo shuleni hapo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa uongozi wa shule hiyo ulipinga azma hiyo ya wanafunzi
 kuacha shule na kurejeshewa fedha zao.
Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed aliwataja
 washtakiwa hao wanaosoma kidato cha tatu kuwa ni Amosi Shirima (22) na
 James Athuman (22).
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Machi 17 mwaka huu.
Mohamed alidai kuwa siku ya tukio, saa  5:00 asubuhi, washtakiwa hao kwa pamoja
 walimvamia mkuu wa shule, aliyetajwa kwa jina la Awadh Said wakati akiwa ofisini
kwake shuleni hapo.
Baada ya kuvamia ofisini kwake, watuhumiwa walimshambulia sehemu mbalimbali
 za mwili kwa panga na kusababisha majeraha makubwa.
Masoud alisema baada ya mwalimu kuona anashambuliwa, alipiga kelele za kuomba
 msaada kabla ya watu kujitokeza na kuwakamata watuhumiwa na baadaye kuwapeleka
 kituo cha polisi.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa hali ya mwalimu huyo siyo nzuri na anaendelea kupata
 matibabu hospitalini alikolazwa.
Washtakiwa kwa pamoja wamekana shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
 Mahakama hiyo, Safina Semfukwe.
 Hakimu Semfukwe aliamuru washtakiwa kurudishwa rumande mpaka kesi yao
itakapotajwa Aprili Mosi, 2014.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG