HOTUBA YA RAISI IMEVURUGA MWELEKEO HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo fortnine

Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limesema hotuba
ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wiki iliyopita kuzindua Bunge Maalum
la Katiba, imevuruga mwelekeo wa mjadala wa rasimu bungeni humo.
Aidha, jukwaa limebaini kuwa hotuba hiyo imeleta mgawanyiko
kiitikadi na kimisimamo miongoni mwa wajumbe bungeni, hususan katika
suala la muundo wa serikali na Muungano kwani kuna wanaounga mkono
muundo wa serikali mbili na wengine wakitaka tatu.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti
wa Jukata, Hebron Mwakagenda wakati akizungumza na wanahabari, kuhusu
mwenendo wa bunge hilo.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya
Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba iliundwa na Rais Kikwete, hivyo hakupaswa
kuonyesha msimamo wake kuipinga rasimu hiyo katika baadhi ya maeneo.
“Kitendo cha Rais kutumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuzungumzia
muundo wa serikali mbili hakikuwa sahihi. Ifahamike kuwa kiutafiti
haiwezekani kuwahoji watu wote. Matokeo ya takwimu yaliyotolewa na Tume
ya Jaji Warioba yalikuwa ni ya kisayansi kwani walikusanya maoni kwa
kutumia sampuli, na watu zaidi ya laki tatu walihojiwa,” alisema
Mwakagenda.
Akizungumzia ubishani uliopo baina ya wajumbe juu ya kutumika kwa
kura ya wazi au siri, Mwakagenda alisema kinachopaswa ni kufikia
maridhiano ya kura ipi itumike.
Aidha aliongeza kuwa mwelekeo uliopo sasa bungeni, unaonyesha
kutopatikana kwa katiba mpya, bali ni upotevu wa muda na rasilimali
kwani zimeshatumika Sh bilioni 80 za walipa kodi, tangu mchakato
ulipoanza.
Aliongeza kuwa iwapo bunge hilo litaendelea kujadili mambo yasiyo
na tija, kuzomeana, kubezana na kubishana, Jukata litawaongoza wananchi
kulifunga bunge hilo, kwa kutumia ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
0 comments: