MISAMAHA YA KODI KUFUTWA HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo fortnine

Dar es Salaam. Serikali itawasilisha bungeni rasimu ya maboresho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo itafuta misamaha ya kodi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema jana kwamba mpango huo
unafanyiwa uchambuzi na Serikali na kwamba utawasilishwa katika Bunge la
Bajeti wiki mbili zijazo.
Kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa CUF ambaye pia
ni mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa akipigia kelele
juu ya wingi wa misamaha ya kodi akisema imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa
cha mapato ya Serikali.
Profesa Lipumba alisema hivi karibuni kuwa ili
kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali inatakiwa kufuta kabisa
misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1.8 trilioni ambayo ni sawa na
asilimia tano ya pato la taifa.
Siku tano zilizopita, Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya, wakati akiwasilisha mpango wa Bajeti ya mwaka 2014/15 kwa
wabunge, alisema Serikali imepanga kukamilisha utungwaji mpya wa Sheria
ya VAT.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuongeza
wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuanzisha vyanzo vipya
pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa
kodi.
Katika bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali iliondoa msamaha wa VAT kwa viwanda vya nguo vinavyotumia pamba ya ndani.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya CRC
Sogema ambayo inaishauri Wizara ya Fedha, misamaha chini ya Kodi ya VAT
ilifikia Sh802 bilioni kwa mwaka 2012, wakati jumla ya misamaha yote
ilikuwa Sh1.8 trilioni.
Ripoti hiyo ya mwaka 2013 inasema: “Matokeo ya
utafiti huu muhimu yanapendekeza kuwa kuna ufanisi zaidi kwa nchi
zinazoendelea kujikita zaidi katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji
kuliko kutoa misamaha ya kodi kwa mashirika.”
Jana, Lukuvi alisema: “Serikali ina mpango huo na
hivi sasa rasimu ya VAT bado inaandaliwa na jambo hilo lipo mikononi mwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema hakupatikana jana kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika
maandalizi ya rasimu hiyo.
0 comments: