MAFURIKO::WATU 19 146 WAKOSA MAKAZI HUKO RUFIJI by nasanyo fortnine

Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mwantumu Mahiza
 
Mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Morogoro, na maji yake kukimbilia katika mto Lubada Wilaya ya Fufiji, Pwani, zimesababisha athari kubwa baada ya nyumba  19, 146 kuharibika huku watu 72,817 wakikosa makazi.

Mbali na nyumba kuharibika na watu kukosa makazi, pia daraja ambalo ni kiungo cha vijiji vya Muhoro, nalo limezama na kusababisha watu kutumia boti kuvushwa kwenda upande wa pili.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Khatibu Chaulembo, aliliambia NIPASHE jana kwamba mafuriko hayo yalianza toka mwishoni mwa mwezi uliopita na watu wanne kufariki dunia siku tatu zilizopita.

“Haya mafuriko yameleta athari kubwa na bado yanazidi kuwa makubwa na hali hiyo imeilazimisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kufika katika eneo la matukio ili kujionea hali ilivyo na kuipatia jamii taarifa ya kila wanachokiona katika mafuriko haya,” alisema Chaulembo.

Aliongeza kuwa kutokana na mafuriko hayo kuwaathiri wakulima, halmashauri imeshaomba tani 874 za chakula kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa.
Alisema kuwa chakula hicho  kitatumika kwa mwezi mmoja kwa ajili ya waathirika hao.

Alisema pia halmashauri imetoa boti mbili kwa ajili ya kuwabeba wananchi wanaokwenda maeneo ya Muhoro mjini au vijiJini.

“Watu wote wanaosafiri  kutoa Jiji la Dar es Salaam kwenda Muhoro wanalazimika kuishia njiani kutokana na kuzama kwa daraja la Muhoro ambalo linaunganisha vijiji vyake, lakini halmashauri imetoa boti mbili ambazo watu hujitolea mafuta ili kuwekwa katika hizo boti na kuvusha watu,’’ alisema Chaulembo.

Katika hatua nyingine, Chaulembo alisema kuwa  Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, amewaagiza madiwani wote wa halmashauri hiyo kwenda katika  maeneo yao ili wawe wanatoa taarifa za mafuriko na hatua zinazochukuliwa.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG