DENGUE HOMA TISHIO DAR YAMKUMBA RAY C ISOME HII HAPA by nasanyo fortnine

Miongoni mwa walioathiriwa na homa hiyo ni
mwanamuziki maarufu
Rehema Chalamila (Ray C) ambaye amelazwa katika Wodi
Namba Tano ya Hospitali ya Mwananyamala.

Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, alithibitisha kulazwa kwa Ray C kutokana na ugonjwa huo jana.
“Tumethibitisha kwamba Ray C ana dalili zote za
dengue, lakini kimaadili siruhusiwi kutoa taarifa za mgonjwa,” alisema
daktari huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Hata hivyo, waandishi wa gazeti hili walimwona
mwanamuziki huyo hospitalini hapo akiwa katika usingizi mzito na
madaktari walisema hakuwa katika hali mbaya bali alikuwa amelala kwa
sababu ya uchovu wa dawa.
Mbali na Ray C, pia madaktari watatu na muuguzi mmoja wameripotiwa kuugua ugonjwa huo.
Tayari mamlaka zimetoa tahadhari kwa wananchi
kuwataka wachukue hatua za haraka kuzuia maambukizi ya homa hiyo
inayosababishwa na mbu anayejulikana kitaalamu kama aedes egyptiae.
Hadi sasa wagonjwa zaidi ya 100 wameripotiwa
kuugua ugonjwa huo katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke na baadhi
wakiripotiwa kupoteza maisha.
Takwimu kutoka Kitengo cha Utafiti wa Magonjwa cha
Ifakara (IHI), kilichoweka kambi katika Hospitali ya Mwananyamala
kutafiti aina za homa, zinaonyesha kuwa kwa miezi miwili ya Machi na
Aprili pekee, wagonjwa 85 walibainika kuwa na homa hiyo.
Hata hivyo, idadi inaweza kuwa kubwa zaidi
kutokana na kukosekana kwa takwimu, vipimo na watu kuufananisha ugonjwa
huo na malaria.
Daktari kiongozi wa hospitali hiyo ambaye pia ni
mtaalamu wa ugonjwa huo, Dk Mrisho Rupinda alisema kuwa kuna taarifa za
wagonjwa wa dengue walioripotiwa katika maeneo yote ya Dar es Salaam.
“Katika kipindi cha wiki moja iliyopita tayari
madaktari wawili kwenye hospitali hii wamebainika kuugua ugonjwa huo,
tunahisi walipata maambukizi kwenye maeneo ya humuhumu ndani hospitali,”
alisema Dk Rupinda.
0 comments: