UKAWA WASUSIA KIKAO BUNGENI HABARI KAMILI HII HAPA by nasanyo fortnine

by nasanyo fortnine
 
Dalili  mbaya za Bunge Maalum la Katiba  kuondoka Dodoma bila kutungwa Katiba mpya zimeanza kuonekana, baada ya wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia kikao jana na kutoka nje ya bungeni.

Wajumbe hao wanaounda umoja huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo baada ya kuanza kwa kikao cha jana jioni.

Sababu iliyosababisha kutoka nje kwa wajumbe hao kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa  ni za ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.

Akiwa mjumbe wa nne kuchangia mjadala wa Rasimu ya Katiba sura za kwanza na sita, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa Lukuvi alitoa kauli hiyo Jumamosi iliyopita mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma.

Profesa Lipumba alisema kwamba Lukuvi aliyemwakiisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa mshahara wanajeshi, Jeshi litachukua nchi.

Alisema kuwa kauli hizo zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa na kuundwa katiba moja.

Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini ya dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni Tume iliyoundwa na Rais.

 UBAGUZI

“Na waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda…Mheshimiwa hii inasikitisha na inasikitisha kwa kuwa kauli hii pia inafanana na kauli ambayo Rais Jakaya Kikwete aliitoa wakati akitoa hotuba katika bunge hili,” alisema.

“Hii ni Rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba, lakini katika mjadala wetu hapa umekuwa na utaratibu wa ubaguzi, watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la ‘Intarahamwe’, hii ni hatari kwa nchi yetu,

“Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo, hii hatuitaji katika nchi yetu, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa, bila kujali, rangi zetu, makabila yetu, dini zetu, hii ndiyo nchi aliyotuachia Mwalimu Nyerere,” alisema.

“Kutokana na hali hii, tumechoka kusikiliza matusi, tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Interahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania…hili hatulikubali, hatulikubali, tunawaachia, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia Interahamwe muendelee na kikao chenu,” alisema.

“Hatuwezi kuwa sehemu ya Interahamwe,” alisema Profesa Lipumba na baada ya kumaliza kuzungumza, wajumbe wote wa Ukawa na wengine walisimama na kuondoka ndani ya ukumbi huku wakipiga kelele.

Baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku wajumbe wa kundi hilo linalojumuisha vyama vya hivyo pamoja na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, huku wakiimba nyimbo mbalimbali. “Tunaondoka, tunawaacha Interahamwe, Interahamwe.”

Saa 10: 48 jioni wajumbe hao waliingia katika ukumbi wa Msekwa na kujumuika na viongozi wa kundi hilo, Prof. Ibrahimu Lipumba, Freeman Mbowe na James Mbatia kwa ajili ya mazunguzo yaliyochukua takribani dakika 25.

Akizungumza na wajumbe hao, Prof. Lipumba, aliwapongeza kwa kuitikia wito wa kutoka nje ya ukumbi.

Alisema wameamua kususia mjadala baada ya kubaini kilichokuwa kikiendelea hakina tija kwa wananchi.

“Mambo yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Bunge hayana tija kwa wananchi, hatuwezi kuungana nao kufanya maasi kwa wananchi,” alisema na kuongeza:
“Mchana saa 9:30 tulifanya kikao, lakini waliohudhuria walikuwa wachache, lakini tunashukuru wote mmeitikia wito wa kutoka.”

LUKUVI NA KANISA
Alitaja sababu nyingine iliyowafanya watoke nje ya ukumbi wa Bunge wakati mjadala ukiendelea ni hatua ya Lukuvi kuzungumza ndani ya kanisa, akieleza kuwa ulikuwa ni makakti maalum wa kuwabana Wazanzibari.

Profesa Lipumba aliwataka wajumbe hao kuhudhuria kikao cha pamoja kitakachofanyika leo kwa ajili ya kuweka mikakati ya nini cha kufanya.

“Wana Ukawa tukutane kesho saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kuweka the way forward tukiondoka kwa ajili ya mapumziko ya Pasaka ndiyo moja kwa moja,” alisema.

Kabla ya kufunga kikao hicho, Prof. Lipumba, alitoa fursa kwa mjumbe anayetaka kusema chochote, ambapo Mchungaji Mtikila, alieleza kuwa, alipata taarifa kuwa Lukuvi aliwaambia waumini wakanisa hilo kuwa wanataka muundo wa serikali mbili ili kuwadhibiti Waislamu.

“Hili linakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa uhuru wa kuabudu kwa wananchi, hili ni lazima tulifanyie kazi ni kubwa,” alisema Mchungaji Mtikila.

TUTARUDI IWAPO…
Baada ya kikao hicho, Prof. Lipumba alipoulizwa na waandishi wa habari kama Ukawa wamesusia moja kwa moja Bunge la Katiba, alisema wanaweza kurudi endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika Rasimu iliyopendekezwa na Tume ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali tatu.

MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni hadi Bunge linaahirishwa ngwe ya kwanza, itaathiri upitishaji wa sura hizo kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi kisichozidi siku moja.

Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Ibara ya 3 inasema pale  mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti ya fasiri ya (2).

Ibara ya Nne, endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati ya mashauriano ili kupata muafaka.

Mjumbe mmoja alilisema kuwa kama wajumbe hao watarejea bungeni maamuzi yatakayofanyika yatakuwa vigumu kupita kwa kuwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwepo.

0 comments:

Copyright © 2014 NASANYO BLOG