RUSHWA BUNGENI WAZIRI MKUU AHUSISHWA KWENYE MLOLONGO HUO HABARI KAMILI by nasanyo fortnine
Dar es Salaam. Hali ya hewa jana ilichafuka
kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri
Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya
wajumbe wa kundi la 201.
Katika tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa
Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa
walitoa rushwa ya vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge
mkono msimamo wa serikali mbili.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa
mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma
hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi
hilo walicharuka na kujaribu kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa
iwapo Wenje asingeomba radhi, asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana
(Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani “walilia” sana kuwa
Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha Mapinduzi
kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe wengine 201,
lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi hilo asilimia
80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa kama mganga
wa jadi.
Ingawa hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha
kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi
la waganga wa jadi.
Kuhusu rushwa, Wenje alisema:“…Sasa kuna wajumbe
wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa
wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika usiku. Hii haikubaliki.”
Baada ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe
alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti
Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya
wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu
uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya
kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa
taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia
chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.
“Kwa sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake
mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje aniombe radhi,”
alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira, huku kukiwa na
sauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.
0 comments: