DARAJA LA DUMILA LILILO BOMOLEWA NA MAFURIKO LAKAMILIKA habari kamili iko hapa isome by tuntu baby
WAZIRI wa Ujenzi Dk.John Magufuli (wa pili
kulia), akiruhusu magari kupita katika daraja la Mto Mkundi jana
baada ya matengenezo ya tuta la daraja hilo kusombwa kwa maji kutokana
na mafuriko katika tarafa ya Magole wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Kulia ni Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Morogoro,
Boniface Mbao,
Ili kukamilisha kazi hiyo, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alilazimika kukesha na wataalam wa wizara hiyo kusimamia ukamilishaji ujenzi wa tuta la daraja la muda la mto huo lililoko wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Ujenzi huo ulikamilika jana saa 4.45 asubuhi na magari zaidi ya 5,000 yaliyokuwa yamekwama kuanza kuruhusiwa kupita.
Baada ya kubomoka eneo la barabara hiyo, mabasi na magari madogo yenye uzito wa pungufu ya tani saba, yalitumia barabara ya Melela kuelekea Kilosa hadi Dumila na hadi sasa yanaendelea na njia hiyo.
Malori makubwa yaliyokwama yalianza safari jana kwa kuruhusu lori moja kupita.
Alhamisi wiki hii, Waziri Magufuli alipofika kwa mara ya kwanza katika eneo hilo, alihidi kukesha mpaka ujenzi wa tuta hilo utakapokamilika.
Dk. Magufuli alisimamia ujenzi wa daraja hilo na kuhakikisha kuwa linakamilika ndani ya saa 24 hivyo kurejesha mawasiliano ya barabara kati ya Morogoro na mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Pamoja na Waziri Magufuli, wengine waliokuwamo katika usimamizi huo ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Nyamuhanja, Kaimu Mkurugenzi wa Barabara Ven Ndyamukama, Meneja wa Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) Morogoro, Doroth Mtenga pamoja na wahandisi wa ujenzi wa mikoa ya Dodoma, Pwani na Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya kutembelea eneo la mafuriko Jumatano wiki hii ili kujionea athari za mafuriko hayo, aliahidi serikali itarudisha mawasiliano ya barabara hiyo kesho.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo na kuruhusu magari ya mizigo yaliyokwama kwa siku tatu baada ya mafuriko hayo kuzoa tuta la daraja,Waziri Magufuli alisema alilazimika kukesha kusimamia ujenzi huo ili kuokoa uchumi wa nchi kwani daraja hilo ni kiungo kikubwa kinachounganisha mikoa na nchi jirani.
“ Nyote ni mashahidi hapa haya maji yalikuwa ni balaa, niliwaambia kuwa kesho magari yataanza kupita lakini kuna watu walinibishia na wengine wakaniambia naleta porojo niondoke zangu, lakini si leo tunafungua hii barabara na magari yanapita kama kawaida,” alisema Waziri Magufuli na kushangiliwa na madereva waliokuwa wanalala kulinda shehena na magari yao.
Alieleza kuwa mafuriko hayo yalisababisha kuharibika kwa tuta la daraja lenye mita 50 kwa upande wa Morogoro na mita 20 kwa upande wa Dodoma hali ambayo endapo jitihada zisingechukuliwa barabara hiyo ingeathiri uchumi,
Usafirishaji wa shehena na mafuta kwenda Congo, Zambia, Rwanda na Burundi.
Kazi hiyo ilikuwa imalizike Jumapili kutokana na ugumu wake, lakini wameikamilisha ndani ya saa 24 na hivyo kuanza kupita kwa magari hayo.
Alisema magari yanayopewa kipaumbele ni yale yanayotoka upande wa Morogoro kuelekea Dodoma kwa kuwa ndiyo yenye mizigo ya mafuta na bidhaa nyingine kuelekea mikoa mingine na nje ya nchi.
Aliwataka madereva kuacha kuzidisha uzito uliwekwa wa tani 56 ili kuokoa madaraja na barabara.
Kwa upande wao, madereva wa malori yaliyokwama barabarani walimteua Mwanyekiti Enest Shekif kuwawakilisha katika ufunguzi huo.
Akizungumza alimpongeza Waziri Magufuli kwa jitihada hizo alizofanya na kueleza kuwa ameonyesha kuwa si wa kubahatisha.
“ Nimetumwa na madereva wenzangu zaidi ya 5,000 tuliokwama hapa kwa siku mbili, mwanzoni tulijua hii ni kazi ya wiki ndiyo tutapita na alikuja Waziri Mkuu alisema mpaka Jumapili njia itafunguliwa ,lakini ulipokuja wewe tukawa na imani ni kweli leo tunapita ndani ya masaa 24.”
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alimuomba Waziri Magufuli kwenda kuzungumza na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuipitia mikataba ya madereva wa malori kwani wanawanyonya na kulipwa Sh 150,000 kwa safari wakati mikataba wanayoiwasilisha serikali inaonyesha kuwa wanalipwa 600,000 by tuntu baby
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI...
0 comments: